Majlis Khuddamul Ahmadiyya mkoa wa Dar Es Salaam wameshiriki katika zoezi maalumu la matembezi ya baiskeli na kugawa vipeperushi katika kuadhimisha siku ya Masihi Aliyeahidiwa ambayo hufanyika ifikapo Machi 23 ya kila mwaka.
Matembezi hayo
yaliwashirikisha pia viongozi wa Majlis Mulk ya Khuddamul
Ahmadiyya akiwemo Sadr sahib.
Wakiwa wamevalia vizibao
maalumu (reflectors) zenye ujumbe wa ISLAM FOR PEACE yaani ISLAMU KWA AMANI, msafara
ulianzia Masjid Salaam mnamo saa 3:00 asubuhi baada ya maombi yaliyoongozwa na Amir
na Mbashiri wa Jamaat Ahmadiyya Tanzania, Sheikh Tahir Mahmood Chaudhry, ukiingilia
barabara ya Bibi Titi Mohammed kuelekea barabara ya
Lumumba pamoja na gari mbili, moja iliyotangulia mbele kuongoza na nyingine
ilibaki nyuma kuhakikisha hali usalama kwa waendesha baiskeli wetu.
Kutoka Mtaa wa Lumumba, msafara ulipitia barabara ya Uhuru ambapo zoezi la ugawaji vipeperushi lilifanyika kwa takribani dakika 10 likiongozwa na Sadr Sahib.
Baadae msafara ulisimama katika soko la Karume kisha Keko ambapo watu kadhaa walijitokeza kutaka kujua lengo la msafara wetu ambao kwa muda wote wa safari zilisikia sauti za Takbira na Tashahhud kutoka kwa vijana waliokuwa na hamasa ya aina yake.
Baadae msafara uliendelea ukipita katika barabara ya Changombe, Kilwa Road, Gerezani, Stesheni
na baadae kurejea katika barabara ya Bibi Titi Mohammed yalipo Makao makuu ya
Jamaat.
Kila jambo jema halikosi
changamoto. Moja ya matukio ya kukumbukwa ni kitendo cha askari wa Barabarani
wakishirikiana na Polisi wa Usalama kuusimamisha msafara wa waendesha baiskeli
wetu katika eneo la bandari wakidhani kuwa tulikuwa katika mgomo fulani. Baada
ya mazungumzo ya muda mfupi na viongozi wa Khuddam msafara uliruhusiwa huku
Polisi wakifuatilia nyuma hadi Masjid Salaam kuhakikisha kuwa hapakuwa na
ajenda nyingine yeyote zaidi ya matembezi ya Amani.
Tukio hilo la uendeshaji
baiskeli liliwachukua Khuddam kiasi cha saa moja na dakika 10 ambapo
walikamilisha umbali wa Kilomita 10.73 za kuzunguka katika barabara za manispaa
ya Temeke na Ilala.