JavaScriptSDK

Monday, March 20, 2017

KHUDDAMUL AHMADIYYA WAENDESHA BAISKELI NA KUGAWA VIPEPERUSHI KUAZIMISHA SIKU YA MASIHI ALIYEAHIWA a.s.


Majlis Khuddamul Ahmadiyya mkoa wa Dar Es Salaam wameshiriki katika zoezi maalumu la matembezi ya baiskeli na kugawa vipeperushi katika kuadhimisha siku ya Masihi Aliyeahidiwa ambayo hufanyika ifikapo Machi 23 ya kila mwaka.

Matembezi hayo yaliwashirikisha pia viongozi wa Majlis Mulk ya Khuddamul Ahmadiyya akiwemo Sadr sahib.

Wakiwa wamevalia vizibao maalumu (reflectors) zenye ujumbe wa ISLAM FOR PEACE yaani ISLAMU KWA AMANI, msafara ulianzia Masjid Salaam mnamo saa 3:00 asubuhi baada ya maombi yaliyoongozwa na Amir na Mbashiri wa Jamaat Ahmadiyya Tanzania, Sheikh Tahir Mahmood Chaudhry, ukiingilia barabara ya Bibi Titi Mohammed kuelekea barabara ya Lumumba pamoja na gari mbili, moja iliyotangulia mbele kuongoza na nyingine ilibaki nyuma kuhakikisha hali usalama kwa waendesha baiskeli wetu.




Kutoka Mtaa wa Lumumba, msafara ulipitia barabara ya Uhuru ambapo zoezi la ugawaji vipeperushi lilifanyika kwa takribani dakika 10 likiongozwa na Sadr Sahib.
Baadae msafara ulisimama katika soko la Karume kisha Keko ambapo watu kadhaa walijitokeza kutaka kujua lengo la msafara wetu ambao kwa muda wote wa safari zilisikia sauti za Takbira na Tashahhud kutoka kwa vijana waliokuwa na hamasa ya aina yake.


Baadae msafara uliendelea ukipita katika barabara ya Changombe, Kilwa Road, Gerezani, Stesheni na baadae kurejea katika barabara ya Bibi Titi Mohammed yalipo Makao makuu ya Jamaat.



 Kila jambo jema halikosi changamoto. Moja ya matukio ya kukumbukwa ni kitendo cha askari wa Barabarani wakishirikiana na Polisi wa Usalama kuusimamisha msafara wa waendesha baiskeli wetu katika eneo la bandari wakidhani kuwa tulikuwa katika mgomo fulani. Baada ya mazungumzo ya muda mfupi na viongozi wa Khuddam msafara uliruhusiwa huku Polisi wakifuatilia nyuma hadi Masjid Salaam kuhakikisha kuwa hapakuwa na ajenda nyingine yeyote zaidi ya matembezi ya Amani.

Tukio hilo la uendeshaji baiskeli liliwachukua Khuddam kiasi cha saa moja na dakika 10 ambapo walikamilisha umbali wa Kilomita 10.73 za kuzunguka katika barabara za manispaa ya Temeke na Ilala.


Kitaifa na kimkoa, maadhimisho ya Siku Masihi Aliyeahidiwa na Mwanzilishi wa Jumuiya ya Waisalamu Waahmadiyya Ulimwenguni Hadrat Mirza Ghulam Ahmad a.s yatafanyika katika viwanja vya Jamaat katika eneo la Kitonga siku ya Jumapili.

No comments: