|
Hadhrat MIRZA MASROOR AHMAD (a.t.b.a), Kiongozi wa Kiroho wa Jumuiya Ya Waislamu Waahmadiyya Duniani |
Kwa jina la Mwenyezi Mungu, Mwingi wa Rehema,
Mwingi wa Ukarimu.
Makala ifuatayo ina
maelezo ya itikadi na mafundisho ya Jumuiya ya Waisalmu Ahmadiyya katika Uislamu,
kifafanuzi cha madai ya Mwanzilishi wake Mtakatifu na hoja za msingi wa madai
yake. Makusudio yangu katika kuandika makala haya , msomaji mpenzi, ni
kukufikishia wewe na wengine, Ujumbe ambao Mwenyezi Mungu Ameuleta kwa wanadamu
siku hizi ili kuwakusanya kwenye Uislamu na Mtume Wake Mtakatifu (s.a.w.). Kama
uchukue taabu ya kuzisoma kurasa hizo zote, sio tu kwamba utapata shukurani zangu
nyingi, bali vilevile utajipatia radhi ya Mwenyezi Mungu.
UAHMADIYYA SI DINI MPYA
Kwanza ningependa
kubainisha suala moja kwamba majina Mwahmadiyya, Uahmadiyya n.k., hayaashirii
kwenye dini mpya. Waahmadiyya ni Waislamu na dini yao ni Islam. Kuutoka Uislamu
hatua moja tu wanaamini kuwa ni haramu na kukosa bahati. Naam, Waahmadiyya
wametwaa majina, Uahmadiyya, Mwendeleo wa Ahmadiyya na kadhalika. Lakini kutwaa
jina sio maana yake kuwa ni dini mpya. Majina Mwahmadiyya, Uahmadiyya n.k., yanakusudiwa
tu kuwapambanua Waislamu Waahmadiyya na Waislamu wengine.
UISLAMU ULITABIRIWA
Jina Islam, ni jina
zuri ambalo Mwenyezi Mungu mwenyewe amewapa wafuasi wa Mtukufu Mtume s.a.w. na
ambalo miaka mingi kabla yake lilipata nafasi ya heshima katika bishara za
Manabii wa zamani. Quran Tukufu inasema:
"Yeye aliwaiteni
Waislamu tangu zamani na katika (Quran) hii pia"
(22:79).
Na katika Biblia
imeandikwa:
"Nawe utaitwa
jina jipya litakalotajwa kwa kinywa cha Bwana" .(Isaya 62:2).
Hakuna jina jingine
linaloweza kuwa na baraka zaidi na takatifu kuliko lile ambalo Mwenyezi Mungu
amelivisha heshima kwa kuwafanya Manabii wengine walitabiri. Nani ataliacha
jina hili? Jina hili ni penzi kwetu kuliko maisha yetu. Na dini inayoungana na
jina hili ndicho chanzo cha pekee cha uhai wa kiroho. Lakini kama ilivyo katika
wakati wetu huu, firka (makundi) mbalimbali za Waislamu, kwa sababu ya hitilafu
ya itikadi zao na mwendo, wamejitwalia majina mbalimbali, imetuwia lazima nasi pia
tuwe na jina maalum ili tujipambanuwe katika Waislamu wengine. Jina bora
tuliloweza kutwaa ni jina Mwahmadiyya au Uahmadiyya. Jina hili linalingana na
wakati huu. Huu ndio wakati ulioteuliwa kwa ajili ya kutangazwa dunia nzima ule
Ujumbe wa Kiulimwengu wa Mtukufu Mtume s.a.w. Ndio wakati wa kuenezwa sifa za
Mwenyezi Mungu na kuenezwa Elimu ya Fadhili na Uzuri Wake, ndio wakati wa
kudhihirishwa sifa ya Ahmadiyyat baada ya kudhihirishwa sifa ya Muhammadiyyat.
Hakuna jina zuri lenye kutambulisha siku hizi zaidi ya hili tuliloweza kutwaa. Tu
Waislamu kwa moyo na roho. Tunashika itikadi ambazo Mwislamu wa kweli
inamlazimu kuzishika na tunakana itikadi ambazo Mwislamu wa kweli inamlazimu
kuzikana. Kama licha ya kushiriki kwetu kwa moyo kwenye kweli za Uislamu na
kufuata kwetu amri za Mwenyezi Mungu, mtu yeyote atupe sifa ya ukafiri na
atueleze kama waghushi au waaminio wa dini mpya, ni mtu katili sana.
Atahukumiwa na Mwenyezi Mungu. Mtu anaweza kulaumiwa kwa yale anayoyatangaza
kwa mdomo wake, sio kwa yale yaliyo moyoni mwake. Kwani, nani awezaye kusema
yaliyomo moyoni mwa mwingine? Kama mtu anamshutumu mwenzake kwa kusema jambo
moja na kuamini jingine, anajiinua mwenyewe kwenye cheo cha Mwenyezi Mungu. Ni
Mwenyezi Mungu tu ndiye ajuaye yaliyomo mioyoni mwa watu. Yeye peke yake
anaweza kusema yale afikiriayo mtu na yale anayoamini. Mtukufu Mtume s.a.w. anakubali
ukomo huu wa kibinadamu. Na tena ni nani angeweza kujua moyo wa mtu zaidi
kuliko yeye? Anasema juu yake mwenyewe:
"Miongoni mwenu
kuna wanaoniletea mabishano yao. Mimi ni mtu
kama ninyi.
Inawezekana baadhi yenu wakawa watetezi hodari
kuliko wengine.
Hivyo, kama nikimpa mmoja haki ya mwingine,
nitakuwa ninampa
sehemu ya moto. Ni juu yake kukataa."
(Sahihi
Bukhari,
Kitabul-Ah'kaam Babu Mauizatul-Imam lilikhusuum).
Tunasoma katika Hadithi kwamba Usama
bin Zaid aliteuliwa na Mtukufu Mtume s.a.w. kuwa Amir wa kikosi fulani. Usama alipambana
na kafiri mmoja na kumshambulia. Kafiri huyu alipokaribia kuuawa, alitamka
Kalima, akithibitisha kuamini ukweli wa Dini ya Islam. Hata hivyo Usama
alimwua. Mtukufu Mtume s.a.w. kusikia hivi, akamkaripia Usama. Akijitetea Usama
alisema:
"Oo Mtume wa
Mwenyezi Mungu, alifanya vile kwa woga."
Mtukufu Mtume s.a.w.
akamjibu, "Kwa nini? Je, ulipasua moyo
wake ukauona?
(Masnud, Imam Ahmad bin Hambal).
Elimu ya yale
yapitayo mioyoni mwa watu haikupewa wanadamu. Haikumpasa Usama kudhani kama
Kalima aliyotamka mtu huyu ilikuwa ni matokeo ya woga au la. Kwahiyo, tunaweza
kulaumiwa kwa yale tuyatamkayo, sio kwa yale yanayoweza kudhaniwa kuwa yamo
mioyoni mwetu. Yaliyomo mioyoni mwetu anayajua Mwenyezi Mungu tu. Anayedai
kumlaumu mwenzake kwa yaliyomo moyoni mwake ni mwongo. Yeye anakiuka mipaka
yake na atahukumiwa na Mwenyezi Mungu. Hivyo, sisi wa Jumuiya ya Ahmadiyya
tunapotangaza kuwa tu Waislamu, hapana mwenye haki kusema kwamba Uislamu wetu
ni wa kujisingizia; ya kwamba mioyoni tunakana Uislamu au tunamkana Mtume
Mtukufu s.a.w.; na ya kwamba tuna Kalima mpya au kuelekea Kibla kipya
tunaposali. Kama inaweza kuwa haki kwa wengine kutupa sifa hizi, basi inaweza
kuwa haki kwetu kutoa sifa hizi kwa watu wengine. Tungeweza kusema kuwa tangazo
lao la Uislamu ni kisingizio, kwamba Mungu apishe mbali, wanaukana Uislamu na
kumtukana Mtukufu Mtume s.a.w. wanaporudi majumbani kwao. Lakini hatuwezi
kupotezwa na upinzani. Hatutasema juu ya yeyote kwamba anasema jambo moja na kuamini
jingine; ya kwamba ana jambo moja midomoni mwake na jingine moyoni mwake. Kwa
amri ya Sheria, uamuzi wetu juu ya wengine utafuata yale waliyonayo na
wanayoyatangaza waziwazi.
|
HADHRAT MIRZA NASIRUDDIN AHMAD (RA) KHALIFATUL MASIH III |
ITIKADI ZA WAAHMADIYYA
Sasa ninaendelea kueleza itikadi
zinazoshikwa na Jumuiya yetu ili uone kama kuna yoyote iliyo kinyume na
Uislamu:-
(1) Tunaamini kwamba
Mwenyezi Mungu yupo; kushiriki katikakuamini kuwapo Kwake ni kutangaza ukweli
wa maana sana; sio kufuata mawazo au dhana.
(2) Tunaamini kwamba
Mwenyezi Mungu ni Mmoja. Hana mshirika hapa wala mbinguni. Kila kitu kingine ni
kiumbe Chake na kinategemea msaada Wake. Hana mwana wala binti. Hana baba wala
mama. Hana mke wala ndugu. Ni wa pekee katika Umoja Wake na katika Nafsi Yake.
(3) Tunaamini kwamba
Mwenyezi Mungu ni Mtakatifu, ameepukana na kila upungufu na ni mwenye kila
ukamilifu. Hakuna upungufu unaoweza kuonekana ndani Yake, na hakuna ukamilifu usioweza
kupatikana ndani Yake. Uwezo Wake hauna ukomo. Na ndivyo ilivyo Elimu Yake. Amekizunguka
kila kitu na hakuna kinachomzunguka Yeye. Ni wa Mwanzo na wa Mwisho, Yu Dhahiri
na Amejificha pia. Ndiye Mwumbaji na Mola wa viumbe vyote. Utawala Wake
haujapata kushindwa, haushindwi, na hautashindwa kamwe. Ameepukana na kufa. Ni
Mwenye uhai wa milele. Hapati upungufu wowote. Matendo yake ni ya hiyari Yake,
halazimishwi. Anautawala ulimwengu wote hivi sasa kama alivyokuwa akiutawala
zamani. Sifa Zake ni za milele, Uwezo Wake u dhahiri siku zote.
(4) Tunaamini kwamba
Malaika ni sehemu ya viumbe vya Mwenyezi Mungu. Wanafuata kanuni iliyoelezwa na
Quran Tukufu:
"Wanafanya
wanayoamrishwa" (16:51).
Kwa Hekima Yake wameumbwa
ili wafanye kazi fulani fulani maalum. Kuwapo kwao ni hakika na kutajwa kwao
ndani ya Kitabu Kitakatifu si kwa methali. Wanamtegemea Mwenyezi Mungu kama
wamtegemeavyo wanadamu au viumbe Vyake vingine. Hawategemei wao kwa kudhihirisha
Uwezo Wake. Laiti Angetaka, Angeumba ulimwengu bila Malaika, lakini Hekima Yake
kamilifu ilitaka kuumbwa kwao. Kwa hivi Malaika wakawapo. Mwenyezi Mungu
aliumba nuru kwa ajili ya macho na mkate kwa ajili ya njaa. Aliumba nuru na
mkate siyo kwa sababu alikuwa na haja navyo, la; kadhalika Hakuwaumba Malaika
kwa sababu Anawategemea, bali Malaika wanadhihirishatu matakwa na Hekima ya
Mwenyezi Mungu.
(5) Tunaamini kwamba
Mwenyezi Mungu Anasema na watumishi Wake wateule na kuwafunulia makusudio Yake.
Ufunuo wa Mungu hushuka kwa maneno. Mpokeaji wa ufunuo hatoi maana wala maneno
ya ufunuo. Vyote hutoka kwa Mwenyezi Mungu. Ufunuo unatoa haja hasa ya mtu. Mtu
anaishi kwa huo na kwa njia ya huo mtu anapata kuungana na Mwenyezi Mungu.
Maneno ya ufunuo ni ya pekee katika nguvu na utukufu. Hakuna mtu awezaye kuyatunga
maneno hayo. Yanabeba hazina ya elimu na hekima. Yako kama mgodi ambao
unakunufaisha zaidi ukiendelea kuchimba. Kwa kweli, mgodi si kitu mbele ya
ufunuo. Mgodi unaweza kwisha, lakini sio hekima ya ufunuo. Ufunuo uko kama bahari
yenye ambary kwa juu yake na chini yake kuna lulu za thamani sana. Wale wanaoelekea
bahari wanaburudishwa na manukato, na wale wanaozama wanakuta lulu chini yake.
Ufunuo ni wa namna nyingi. Baadhi ya wakati unaleta amri na Sheria, pengine
maonyo na mawaidha. Baadhi ya wakati unaleta elimu ya ghaibu, pengine hazina za
elimu za kiroho. Baadhi ya wakati unaleta furaha na radhi ya Mwenyezi Mungu,
pengine wajulisha makasiriko Yake, pengine wadhihirisha mapenzi Yake, na
pengine humwelekeza mtu kwenye wajibu wake kwa kumkaripia . Baadhi ya wakati
unafundisha tabia njema za ndani na pengine unaleta elimu Yake juu ya mwendo mbaya
uliojificha wa mtu. Kwa ufupi, itikadi yetu ni kwambaMwenyezi Mungu anaeleza
matakwa Yake kwa watumishi Wake. Maneno haya ni mbalimbali kwa watu wa vyeo na
hali mbalimbali na huwa ya namna nyingi. Katika maneno yote ya Kiungu, yaliyokamilika
zaidi na bora zaidi ni maneno ya Quran Tukufu. Sheria iliyoelezwa na Quran
Tukufu na mwongozo wa kiroho uliomo ndani yake ni wa milele. Hautabatilishwa na
ufunuo wowote
mwingine wa Mwenyezi
Mungu.
(6) Tunaamini kwamba
giza linapoenea ulimwenguni na wanadamu kuzama kwenye madhambi, zama ambazo
bila msaada wa Mungu inawawia shida kujifungua kamba za Shetani, kwa huruma
Yake nyingi na Rehema isiyokadirika, Mwenyezi Mungu Huteua kutokana na
watumishi Wake wapenzi na watiifu, wale ambao anawapa kazi ya kuuongoza
ulimwengu. Mwenyezi Munguanasema katika Quran:
"Na hakuna taifa
lolote ila alipita humo Mwonyaji (Sura 35:25).
Ina maana kwamba
Mwenyezi Mungu alituma Wajumbe Wakekwa watu wote ulimwenguni. Maisha yao safi
na mfano wao mkamilifu ukafanya kazi daima kama mwongozo kwa wanadamu wengine.
Wale wanaowapa migongo, wanajishusha. Wale wanaowaelekea wanajipatia radhi ya
Mwenyezi Mungu. Wanafunguliwa milango ya baraka Zake. Rehema Yake inawafunika.
Wanakuwa waalimu wa kiroho kwa vizazi na vizazi na wanafikia ukuu katika Akhera
na dunia. Tunaamini pia kwamba Mitume wa Mwenyezi Mungu ambao toka zamani
wamewasaidia wanadamu kuwatoa kwenye giza la madhambi, walikuwa wa daraja
mbalimbali za ukuu wa kiroho na walitimiza kwa kadiri mbalimbali makusudio ya
kutumwa kwao. Mkuu wa hao wote alikuwa Mtukufu Mtume Muhammad s.a.w. Mwenyezi
Mungu alimwita mfalme wa wanadamu naye ni:
"Mjumbekwa
wanadamu wote" (34:29).
Mwenyezi Mungu
alimfunulia elimu ya mema na mabaya na akambariki kwa msaada Wake. Wafalme wenye
nguvu sana ardhini waligwaya kwa kumwogopa. Ardhi yote ikawa mahali pa kuabudia
kwa ajili yake (Sahihi Bukhari: mlango wa Tayammum). Wakati ulifika ambao
wafuasi wake walionekana dunia nzima; kila sehemu ya dunia kulikuwa waaminio
walioinama na kumsujudia Mwenyezi Mungu Mmoja, Mungu asiye kifani. Uadilifu
ukaanza kutawala mahala pa batili, huruma mahala pa ukatili. Kama Manabii wa
zamani wangeishi wakati wa Mtume s.a.w., wangelazimika kumtii na kumfuata Nabii
huyu mkamilifu. Quran Tukufu imesema kweli:
"Na (Kumbukeni)
Aliposhika Mwenyezi Mungu ahadi kwa
Manabii: Nikiisha
wapeni Kitabu na hekima, kisha awafikieni
Mtume msadikishaji wa
yale yaliyo pamoja nanyi, ni juu yenu
kumwamini na
kumsaidia" (3:82).
Mtume s.a.w. mwenyewe amesema:
"Lau kama Musa
na Isa wangekuwa hai wasingekuwa na njia ila
kunifuata"
(Tafsir
Ibn Kathir, Kitabu
cha 2, uk. 246).
(7) Tunaamini kwamba
Mwenyezi Mungu anasikia maombi ya watumishi Wake wanaomwomba. Anawaondolea
shida zao. NiMungu aliye Hai, na Uhai Wake u dhahiri katika mambo yote wakati wote.
Mwenyezi Mungu si kama jengo tujengalo tunapochimba kisima ambalo hubomolewa
baada ya kuchimbwa kisima. Bali Yeye ni kama nuru na pasipo Yeye hatuoni
chochote; ni kama roho ambaye akiondoka kila kitu kitakufa. Akiondolewa Yeye na
tuwe mara kama makundi yasiyo na uhai. Sio kweli ya kwamba Mwenyezi Mungu aliumba
ulimwengu kishapo akaenda kukaa pembeni. Anaendelea kutoa ukarimu Wake na
kufungamana na viumbe Vyake. Wanapojiona wanyonge na wadhaifu, anawageukia kwa
msaada Wake. Kama wakimsahau, anawakumbusha juu ya dhati Yake. Ndipo kwa njia
ya Mtume Wake anawathibitishia:
"Basi hakika
Mimi Nipo karibu. Nayaitikia maombi ya mwombaji
anaponiomba, basi
waniitikie na waniamini, ili wapate kuongoka"
(2:187).
Yaani, Mwenyezi Mungu
anasikia maombi ya watu Wake. Ni juu yao kumwamini na kumwomba Yeye. Kama
wakifanya hivi, bila shaka atawaongoza.
(8) Tunaamini kwamba
kwa zama mbalimbali Mwenyezi Mungu hupanga kutokea kwa matukio kwa njia maalum.
Matukio ya duniani hayafanyiki kwa kanuni za asili peke yake. Bali, mbali na
kanuni hizi kuna kanuni maalumu ambayo kwayo Mwenyezi Mungu hudhihirisha Uwezo
Wake, Utukufu Wake na Kudra Yake.Ndiyo Kudra ya Mwenyezi Mungu ambayo baadhi ya
watu kwa
ujinga wao wanaikana.
Watu kama hao hawaamini chochote ghairi ya kanuni za asili. Naam, kanuni za
asili ni za asili tu lakini sio kanuni za Kudra ya Mwenyezi Mungu. Kanuni za
Kudra ya Mwenyezi Mungu ni kanuni ambazo kwazo Mwenyezi Mungu huwasaidia
wateule Wake, wale anaowapenda; kwa hizo anahilikisha na kufedhehesha maadui wa
rafiki Zake. Kama hakungekuwa kanuni hizi, Musa, aliyekuwa dhaifu na mnyonge angewezaje
kumshinda Firauni aliyekuwa mfalme jabari na katili? Ingewezekanaje Musa kushinda
na Firauni kushindwa ambapo Musa alikuwa dhaifu na Firauni alikuwa mwenye
nguvu? Kama hakuna kanuni ghairi ya kanuni za asili, ni kwa vipi Mtukufu Mtume Muhammad
s.a.w. angeweza kuishinda Bara Arabu iliyoamua kumwua na kufuta kabisa kazi
yake. Katika kila pambano, Mwenyezi Mungu alimsaidia Mtukufu Mtume s.a.w. na
kumpa ushindi juu ya maadui zake. Kila shambulio walilofanya maadui liliishia
kwa kushindwa kwao, na hatimaye, baada ya miaka kumiya kuuhama mji wa Makka
alipokuwa na Sahaba mmoja tu aliyejitoa maisha yake kwa kumlinda Mtume,
aliuingia tena mji wa Makka akiwa na Watakatifu elfu kumi. Je, kanuni za asili
zinaweza kutoa matukio hayo? Je, zinaweza kuruhusu mambo hayo? Kanuni za asili
zinadhamini tu ushindi wa mwenye nguvu dhidi ya dhaifu; na kushindwa kwa dhaifu
mbele ya mwenye nguvu.
(9) Tunaamini kwamba
mauti sio mwisho wa kuwapo kote kwa wanadamu. Mwanadamu anaishi baada ya mauti
na kulipwa matendo yake katika Akhera. Wale watendao matendo mema wanapata
malipo ya ukarimu. Wale wanaoasi mafundisho Yake na amri Zake wanakutana na
adhabu iliyo ni haki yao. Hakuna kinachoweza kuzuia hesabu hii. Wanadamu lazima
waishi na kukutana nayo. Mtu anaweza kuchomwa mpaka akawa majivu na majivu
yapeperushwe hewani; anaweza kuliwa na mnyama au ndege au wadudu au ageuke kuwa
mavumbi na mavumbi yageuke kitu kingine hata hivyo ataishi tu baada ya mauti na
kukutana na Mwumba wake na kutoa maelezo ya matendo yake. Uwezo wa Mwenyezi
Mungu unadhamini jambo hili. Sio lazima kwamba mwili
huu uwepo ndipo roho
iwe hai. Mwenyezi Mungu anao uwezo wa kuhuisha mwanadamu kutokana na chembe
chembe ndogo sana za mwili wake au sehemu nyembamba ya roho yake. Hivi ndivyo itakavyokuwa.
Mwili unaweza kugeuka kuwa majivu lakini si lazima yawe si chochote na
kutoweka. Hata roho haiwi hivyo bila idhini ya Mwenyezi Mungu.
(10) Tunaamini kwamba
makafiri na maadui wa Mwenyezi Mungu, mpaka wasamehewe na Mwenyezi Mungu kwa
Rehema Yake kubwa, wataishi mahala paitwapo Jahannamu. Joto kali na baridi kali
vitakuwa ndiyo adhabu za mahala hapo, lakini makusudio hayatakuwa kuwaumiza
wadhalimu, bali kuwasuluhisha. Huko Motoni, makafiri na maadui wa Mwenyezi
Mungu watatumia siku zao kwa mayowe na maombolezo, wakijutia siku walizotumia
kwa kufanya maasi. Wataendelea hivi, mpaka Rehema ya Mwenyezi Mungu, ambayo
imevizunguka vitu vyote, itakapowazunguka waasi na maasi yao. Hapo ndipo ahadi
ya Mwenyezi Mungu iliyotangazwa na Mtukufu Mtume s.a.w. itakapotimia:
"Zama zitaifikia
Jahanamu ambapo hamtakuwa yeyote ndani yake;
pepo zitavuma na madirisha yatapiga
kelele nyingi"
(Tafsir Ma'alim-ut-Tanziil
chini ya Aya 107, Sura Hud).
(11) Tumaamini kwamba
wale wanaomwamini Mwenyezi Mungu na Mitume Wake, Malaika Wake na Vitabu Vyake;
ambao wanafuata, kwa mioyo yao na roho zao, mwongozo utokao Kwake; ambao
wanatembea kwa unyenyekevu na wanajinyenyekeza mbeleYake; wale ambao wanaishi
kama maskini ijapokuwa wawe matajiri; ambao wanawatumikia wanadamu na kujinyima
starehe yao kwa ajili ya wengine; ambao wanaacha kila namna za dhuluma, ukatili
na uhaini; ambao ni mifano ya wema kwa wanadamu na kujitenga na tabia mbaya;
watu hawa watakwenda mahala paitwapo Jannah. Amani na furaha zitaenea mahala
hapo. Hakutakuwa na maumivu. Kila mtu atajipatia furaha na radhi ya Mwenyezi
Mungu. Mungu atakuwapo mbele ya wote, fadhili Zake zitamzunguka kila mmoja.
Watakuwa karibu sana na Mwenyezi Mungu hivi kwamba kila mmoja atakuwa kama kioo
akiangaza kwa Mwenyezi Mungu na sifa Zake kamilifu. Matamanio yote ya ovyo ya
mtu yatatoweka. Matamanio ya watu yatakuwa matamanio ya Mwenyezi Mungu. Watakuwa
wamefikia uzima wa Milele, kila mmoja akiwa mdhihirishaji wa Mwumba Wake.
Hizi ndizo itikadi
zetu. Kama kuna itikadi zingine zozote ambazo mtu lazima awe nazo kabla ya
kusemwa kuwa ni Mwislamu, sisi hatuzijui. Maimamu wa Kiislamu hawaelezi itikadi
zaidi ya hizi. Tunaamini itikadi zote za Kiislamu na kuzishika kuwa itikadi
zetu.
TOFAUTI NA WAISLAMU WENGINE
Sasa, msomaji mpenzi,
unaweza kuanza kustaajabu kwa nini tunafikiriwa kuwa tofauti, tunapoamini kwa
moyo wote itikadi zote zinazojulikana za Uislamu? Kwa nini Maulamaa
wanatutukana? Kwa nini wanatuita makafiri?
Kwa kujibu, ninaweza tu kutaja mambo ambayo kwayo Maulamaa wanasema
tumeutoka Uislamu. Mwenyezi Mungu Akulinde na maoni ya kosa na Akufungulie
milango ya Rehema Zake!
NABII ISSA ALIKUFA KAMA KAWAIDA
Jambo la kwanza na
kubwa kabisa ambalo maadui zetu wanatupinza kwalo ni kwamba sisi tunasadiki
kwamba Nabii Isa (a.s.) wa Nazareti alikufa kifo cha asili. Kusadiki kwamba
NabiiI sa alikufa kifo cha asili kunasemwa ni kumtusi Nabii Isa, ni kuiacha
Quran Tukufu na fundisho la Mtukufu Mtume s.a.w. Ni kweli kuwa tunasadiki kufa
kwa Nabii Isa. Lakini si kweli kwamba kusadiki kuwa amekufa ni kumtusi au
kuacha Quran Tukufu au kuwa mbali na fundisho la Mtukufu Mtume s.a.w. Mtu
akifikiri zaidi juu ya jambo hili mara moja atagunduwa kwamba lawama
tunazolaumiwa sisi hazitokani na itikadi yetu juu ya kifo cha Nabii Isa. Bali zinatokana
na itikadi yao kwamba Nabii Isa hakufa bali yu mzima mbinguni.
|
HADHRAT MIRZA BASHIRUDDIN MAHMOOD AHMAD (RA) Khalifatul Masih II |
Tu Waislamu, na
tukiwa Waislamu wajibu wetu wa kwanza ni kuthibitisha Ukuu wa Mwenyezi Mungu na
heshima ya Mtukufu Mtume s.a.w. Naam, tunawaamini Manabii wote wa Mwenyezi Mungu.
Lakini mapenzi yetu na heshima yetu kwa Mtukufu Mtume s.a.w. ni ya juu sana,
kwa sababu yeye alijitolea kwa ajili yetu; alijikaribishia mauti kwa kutuokoa
na kifo cha kiroho; alihuzunika sana kwa ajili yetu. Aliacha starehe yake kwa
ajili yetu. Alijishusha
ili sisi tusimame
juu. Alipanga namna za manufaa yetu na kutuombea starehe za daima. Aliacha
miguu yake ivimbe kwa kusimama ibadani. Akiwa mtakatifu, aliomba tutibiwe
madhambi yetu, kutuokoa katika Moto; alisali mpaka msala ukaloa kwa machozi.
Alilia mpaka kifua chake kilitoa sauti kama birika la
maji yanayochemka. Kwa
ajili yetu alisogeza Huruma ya Mwenyezi Mungu;
alitaabika kwa
kumpendeza Yeye na kutusaidia sisi pia. Alitufanya tufunikwe na shuka ya Rehema
Yake, kawa la Huruma Yake. Alijitahidi na akapata njia ambazo kwazo tuweze
kumridhisha Mwenyezi Mungu; njia ambazo kwazo tuweze pia kuungana naye. Aliyoyafanya
kwa ajili yetu hayajapata kufanywa kabla na Nabii yeyote kwa ajili ya kaumu
yake. Basi, fatwa za ukafiri zinatupendeza sisi. Tungependa kuitwa makafiri
kuliko kumfahamu Nabii Isa kuwa sawa na Mungu Mwumba wetu, Mruzuku wetu na
Mlinzi wetu, ambaye anatupa mkate wetu wa kila siku na elimu na mwongozo
tunaotegemea kwa
starehe yetu ya
kiroho. Fatwa za ukafiri zinakaribishwa mno nasi kuliko kusadiki kwamba Nabii
Isa yuko hai mbinguni bila ya kula wala kunywa. Tunamheshimu Nabii Isa. Lakini
kwa nini? Kwa sababu ni Nabii wa Mungu wetu. Twampenda Masihi. Lakini kwa nini?
Kwa sababu Mungu alimpenda naye alimpenda Mungu. Kumheshimu kwetu ni kwa sababu
ya kumheshimu Mwenyezi Mungu. Tunawezaje kumweka juu ya Mwenyezi Mungu na kumdharau
Mungu kwa sababu yake? Je, tuwape nguvu wahubiri wa Kikristo ambao kazi yao
kila siku ni kutafuta makosa katika Uislamu na Quran Tukufu? Je, tuwafanye
wafikiri kwamba Nabii Isa alikuwa Mungu? Kwani, kama hakuwa Mungu, anawezaje
kuwa hai mbinguni? Tunawezaje kwa vinywa vyetu wenyewe, kusema jambo livunjalo
heshima ya Umoja wa Mwenyezi Mungu? Tunawezaje kuiharibu na kuangamiza dini
Yake? Maulamaa wako huru kufanya watakalo; wanaweza kuwachochea watu dhidi
yetu, watupige mawe au watuue. Hatuwezi kumwacha Mwenyezi Mungu kwa ajili ya
Nabii Isa. Tungekubali mauti kama tungelazimishwa kusema kwamba Nabii Isa yuko
hai mbinguni kama Mungu – Nabii Isa ambaye Wakristo wanaamini kuwa ni mwana wa
Mungu na ambaye kwa ajili yake wanautupa Umoja na Kujitegemea kwa Mwenyezi
Mungu. Laiti tungebakia ujingani, ingelikuwa vingine.
Lakini tangu macho
yetu yafumbuliwe na Mtume wa Mwenyezi Mungu, ambaye ametuonesha Umoja wa
Mwenyezi Mungu, na Utukufu Wake, na Uwezo Wake, na Ukuu Wake na ukarimu Wake hatuwezi
kufanya hivyo. Na litokee lolote, hatuwezi kumwacha Mwenyezi Mungu kwa sababu
ya kiumbe mwanadamu. Kama tufanye hivi, hatujui tutakuwa wapi. Heshima ni ya
Mwenyezi Mungu na vyeo vyote vinatoka Kwake. Tunapoona waziwazi kwa kusadiki
kuwa Nabii Isa yuko mbinguni ni kumtusi Mwenyezi Mungu, hatuwezi kusema ya kuwa
itikadi hii ni kweli. Sisi hatuwezi kuelewa kwa nini kusadiki kifo cha Nabii
Isa ni kumtusi Isa. Mitume wakubwa wakubwa kuliko Nabii Isa wamekufa na vifo
vyao havikuleta fedheha kwa ajili yao. Vilevile kifo cha Isa hakiwezi Kuwa
fedheha kwake. Lakini kama, kudhania yasiyowezekana, tukutanishwe na mawili -
Mungu au Isa - na kama tutakiwe kufanya uchaguzi, bila shaka tutamchagua
Mwenyezi Mungu. Tuna hakika kuwa Nabii Isa mwenyewe, ambaye alimpenda sana
Mwenyezi Mungu, asingekubali kamwe cheo kinachomheshimisha Isa na kumdharaulisha
Mwenyezi Mungu na Umoja Wake. Quran Tukufu inatufundisha hivihivi:
"Masihi hatebeua
kuwa mtumishi wa Mwenyezi Mungu wala
Malaika
waliokurubishwa" (4:173).
QURAN NA HADITHI VINASEMA NABII ISA KAFA
Tunafungwa hapa na Neno la Mwenyezi
Mungu. Tunaposoma katika Quran Tukufu:
"Na nilikuwa
shahidi juu yao nilipokuwa kati yao, lakini
Uliponifisha Wewe
Ukawa Mchungaji juu yao, na Wewe ni Shahidi
juu ya kila
kitu" (5:118).
Mwenyezi Mungu katika
jina la Nabii Isa anatangaza kwamba Wakristo walipotea baada ya kifo cha Isa.
Alipokuwa hai, walishika imani safi. Kwa kusoma haya ndani Ya Quran, tunawezaje
kufikiri kuwa Isa si mfu bali yu mzima mbinguni? Pia tunasoma ndani ya Quran
Tukufu:
"Ewe Isa, kwa
yakini Mimi Nitakufisha na Nitakuinua Kwangu,
na Nitakutakasa na
(masingizio ya) wale waliokufuru, na
Nitawaweka wale
waliokufuata juu ya wale waliokufuru mpaka
siku ya Kiyama"
(3:56).
Nabii Isa aliinuliwa
kwa Mwenyezi Mungu baada ya kifo chake. Maneno "Nitakuinua" au
"Nitakunyanyua"
yanakuja baada ya maneno "Nitakufisha". Ni lazima
tufuate kanuni za lugha. Linalotajwa mwanzo, lazima litendeke kwanza. Lakini
pengine Maulamaa wanajua kanuni hizi vizuri zaidi kuliko Mwenyezi Mungu. Huenda
wanafikiri kuwa ijapokuwa "Nitakuinua" imetajwa mwisho katika aya
hii, lakini ingetajwa mwanzo. Lakini Mwenyezi Mungu ni Mwenye hekima kinyume na
maarifa yetu. Anajua vizuri mno namna gani mawazo yanatakiwa yaelezwe. Katika
usemi Wake hakuwezi kuwa na kosa, wala kupotoka neno moja katika mpango wa
maneno Yake. Ni Mwumba wetu nasi ni viumbe Vyake.
Tutathubutuje kuona
kosa katika usemi Wake? Lakini Maulamaa wanaonekana kufikiri kwamba kunaweza
kuwa na kosa katika usemi wa Mwenyezi Mungu na sio katika wao kuelewa usemi
huo. Sisi hatuwezi kusema hivi; kwani, tunaona ni maangamio matupu fikara hii. Hali
tuna macho, hatuwezi kutumbukia shimoni. Hali tunajua, hatuwezi kunywa kikombe
cha sumu. Baada ya Mwenyezi Mungu, tunampenda Mtukufu Mtume Muhammad s.a.w. tu.
Ni Mkuu wa Manabii wote. Hakuna mwanadamu mwingine, awe nabii au la, ambaye
amefanya hata sehemu ndogo sana ya yale aliyoyafanya Mtukufu Mtume s.a.w. kwa
ajili yetu. Hatuwezi kumheshimu zaidi mtu mwingine. Haiwezekani kwetu kufikiri
kwamba Isa, Masihi, yu hai mbinguni hali Muhammad, Mtume wetu Mtukufu, amezikwa
chini ya ardhi. Hatuwezi kufikiri hivyo. Tunasadiki kwamba kwa daraja ya
kiroho, Mtukufu Mtume s.a.w. amesimama juu sana kuliko Isa. Inawezekana kweli
Mwenyezi Mungu ampandishe Isa mbinguni kwa sababu ya alama ndogo sana ya hatari
kwa maisha yake, lakini asimpandishe Mtukufu Mtume s.a.w. walau karibu ya nyota
alipokuwa akifukuzwa na maadui zake huku na huko? Hatuwezi kusadiki kwamba
bwana wetu yu mfu ardhini lakini Isa yu hai mbinguni. Tunaona kifo ni afadhali
kuliko imani hii ambayo ni fedheha mbele ya Wakristo. Lakini, mshukuru Mwenyezi
Mungu, mambo hayako hivyo. Mwenyezi Mungu hangeweza, na kwa kweli, hajapata
kumfanyia Mtukufu Mtume s.a.w. namna kama hii. Mwenyezi Mungu Ndiye Bwana wa
mahakimu wote. Yeye Mwenyewe alimwita Mtukufu Mtume s.a.w. kama Mfalme wa
wanadamu, hangeweza kumjali zaidi Isa. Kwa ajili ya Mtukufu Mtume s.a.w.
Mwenyezi Mungu aliutikisa ulimwengu wote. Yeyote aliyefikiri kumfedhehesha, alifedheheka
mwenyewe. Je, angeweza kumfedhehi Mtukufu Mtume s.a.w. na kuwapa maadui nafasi
ya kuchekelea fedheha yake? Kufikiri kuwa Mtukufu Mtume s.a.w. yu mfu ardhini
na Isa wa Nazareti yu hai mbinguni, kunanisisimua nywele. Ninaona ni kiroja na
fedheha pia, kwa hiyo ninajiona nikitangaza "La, Mungu hawezi kufanya
hivi". Anampenda Mtukufu Mtume s.a.w. kuliko yeyote mwingine. Hangeweza
kumwacha afe na kuzikwa lakini ampandishe Isa mbinguni. Laiti mtu yeyote
angestahiki kuwa hai na kupanda
|
HADHRAT MIRZA TAHIR AHMAD (RA), Khalifatul Masih IV |
mbinguni huyo
angekuwa Mtukufu Mtume s.a.w. Kama amekufa kama kawaida, basi Manabii wengine
wamekufa kama kawaida. Hali ya kujua cheo kikubwa sana alichonacho Mtukufu
Mtume s.a.w. mbele ya Mwenyezi Mungu, hatuwezi hata kidogo kufikiri kwamba angefanyiwa
na Mungu Mwenyezi duni ya yale aliyofanyiwa Isa. Hatuwezi kufikiri kwamba zama
za Hijra, Mtukufu Mtume s.a.w. alipojificha ndani ya pango la Thaur, ambalo ili
alifikie ilimbidi abebwe na Seyidna Abubakar r.a., Mwenyezi Mungu hakupeleka Malaika
wowote kumwokoa; lakini Mayahudi walipotaka kumkamata Isa, Mungu akamnyanyua
mpaka mbingu ya nne ili kumwokoa na mpango wa Mayahudi wa kumwua. Katika vita
ya Uhud, Mtukufu Mtume s.a.w. alibakiwa na Waislamu wachache tu waliomzunguka
alipokuwa akishambuliwa na maadui. Mungu hakupeleka Malaika wowote, wala
hakuumba pale zingaombwe ili maadui walishambulie badala ya kumshambulia
Mtukufu Mtume s.a.w., na kuvunja meno ya zingaombwe hilo badala ya meno ya Mtukufu
Mtume s.a.w. Mwenyezi Mungu aliwaacha maadui wamshambulie Mtukufu Mtume s.a.w.
mwenyewe na mpaka alipoanguka kama aliyekufa, maadui wakapiga kelele za shangwe
na hoihoi kwamba (Mungu apishe mbali). wamemwua Muhammad, Mtume wa Mungu.
Lakini kwa kumhusu Isa, Mungu hakuacha hata maumivu kidogo tu yamsumbue. Mara
tu Mayahudi walipoamua kumkamata, Mungu akamnyanyua mbinguni, na mahala pake, wakamkamata
mmoja wa maadui zake ambaye Mungu alimfanya awe na sura ya Isa, na hivyo wakamwamba
msalabani huyu badala ya kumwamba Isa! Tunastaajabu juu ya matokeo ya watu
hawa. Upande mmoja wanadai kumpenda sana Mtukufu Mtume s.a.w.; na upande mwingine,
wenyewe wanaelekea kumdhararu na kumfedhehesha. Na hawakomei hapo. Wanaendelea
mbele na kutoa Fatwa za ukafiri kwa wale ambao kwa sababu ya kumpenda Mtume
s.a.w. wanakataa kushiriki kwenye zile itikadi zinazomweka mtu mwingine juu ya Mtukufu
Mtume s.a.w. Tunashangaa wana muradi gani kwa ukafiri? Je, kufikiri kuwa
Mtukufu Mtume s.a.w. ana daraja ya juu zaidi ya Manabii wengine na kumtolea
heshima inayomstahiki ni ukafiri? Kama huu ni ukafiri, basi Wallahi ukafiri
wetu una thamani mara nyingi zaidi kuliko imani ya wale wanaotupa ukafiri huo.
Seyidna Mirza Ghulam Ahmad, Masihi Aliyeahidiwa, alisema sawa:
"Baada ya
Mwenyezi Mungu, nimelevywa na mapenzi ya
Muhammad. Kama hii ni
kufuru, Wallahi, mimi ndiye kafiri
mkubwa wa makafiri
wote".
Ni lazima sote tufe
siku moja na kusimama mbele ya Mwenyezi Mungu na kujibu tutakayoulizwa. Kwa
nini tumwogope mwanadamu yeyote? Wanadamu wanaweza kutupa dhara gani? Tunamwogopa
Mwenyezi Mungu tu na tunampenda Yeye tu. Baada Yake, tunampenda na kumheshimu
Mtukufu Mtume s.a.w. zaidi. Kama kwa ajili ya Mtukufu Mtume s.a.w. italazimu
kutoa heshima yetu, manufaa na vitu vya dunia hii, tutaona rahisi sana. Lakini kumdharau
Mtukufu Mtume s.a.w. hatuwezi kuvumilia hata kidogo. Hali ya kujua utakatifu
aliokuwa nao, elimu ya kiroho aliyokuwa nayo na ukaribu aliokuwa nao na
Mwenyezi Mungu hatuwezi kufikiri kwamba Mwenyezi Mungu alimpenda mtu mwingine
yeyote zaidi kuliko alivyompenda Mtukufu Mtume s.a.w. Kama sisi tuchukue fikara
hii, tutastahiki adhabu zaidi kuliko wengine wote. Tunajua vizuri sana kwamba
waliomkataa Mtukufu Mtume s.a.w. walimwambia wakimtaka aoneshe mwujiza wa
kupanda mbinguni.
Walisema:
"Au upande
mbinguni; na hatutaamini kupanda kwako mpaka
ututeremshie kitabu
tukisome" (17:94).
Kwa kujibu ombi lao
hili, Mwenyezi Mungu hakumpa Mtume s.a.w. uwezo wa kuonesha mwujiza aliotakiwa
kuuonesha. Badalayake, Mwenyezi Mungu alimwambia Mtukufu Mtume s.a.w.:
Sema: Mola wangu ni
Mtakatifu! mimi siye ila ni mtu tu, Mtume"
(17:94).
Lakini, Maulamaa
wanavyofundisha, Nabii Isa, MwenyeziMungu alimpandisha mbinguni. Mtukufu Mtume
s.a.w. anapoombwa kupanda mbinguni, kupanda mbinguni kunasemwa na Mwenyezi Mungu
kuwa hakuwezekani na mwanadamu. Lakini Isa anapandishwa mbinguni bila haja hata
kidogo. Kama hili ni kweli, je, haitakuwa kwamba Isa hakuwa mwanadamu bali
Mungu? Mungu atulinde na mawazo haya. Je, haitaleta maana kwamba Isa alikuwa na
daraja ya juu zaidi na alipendwa na Mungu zaidi kuliko Mtukufu Mtume s.a.w.?
Lakini tunajua, na ni dhahiri kama jua, kwamba Mtukufu Mtume s.a.w. ni m'bora
na mkuu wa manabii wote. Hali ya kujua hivi, tunawezaje kufikiri kwamba Mtukufu
Mtume s.a.w. hakupanda mbinguni, bali alikufa na kuzikwa ardhini kama kawaida,
lakini Isa apae mbinguni na kuwa huko hai kwa miaka mamia na mamia? Sio tu
kwamba ni jambo la ghera juu Ya Mtume s.a.w. Bali ni jambo la ukweli wake pia,
ukweli wa madai yake. Je, hakusema Mtume s.a.w. kwamba:
"Lau kama Musa
na Isa wangalikuwa hai,
wasingekuwa na njia
ila kunifuata?" (Zurqani, Kitabu cha 6 uk. 54).
Kama Isa yu hai, basi
madai haya ya Mtukufu Mtume s.a.w. ni lazima yasemwe kuwa ni ya uongo. Maneno
ya Mtukufu Mtume s.a.w. yana maana sana na yako dhahiri. Anasema, "Lau
kama" Musa na Isa wangalikuwa hai. Hii "Lau kama"
inawaweka Musa na Isa pamoja na ina maana kwamba hawa wawili ni wafu. Musa si mzima
wala Isa si hai. Hili ni tangazo la maana sana la Mtukufu Mtume s.a.w. Baada ya
kusikia tangazo hili, hakuna mfuasi wa kweli wa Mtukufu Mtume s.a.w. anayeweza
kufikiri kwamba Isa yu hai mbinguni. Maana kama Isa yu hai mbinguni, tangazo la
Mtukufu Mtume s.a.w. linageuka kuwa la uwongo; pia elimu yake juu ya jambo
lenyewe. Kuna tamko jingine la maana sana la Mtukufu Mtume s.a.w. Wakati wa
ugonjwa wake wa mwisho, alimwambia binti yake Fatima:
"Hakika Jibrili
alikuwa akinisomea Quran mara moja kila mwaka.
Na mwaka huu
amenisomea mara mbili. Na akaniambia kuwa kila
Nabii aliishi nusu ya
umri wa Nabii aliyemtangulia. Akaniambia
pia ya kuwa Isa bin
Mariamu aliishi miaka 120. Kwa hiyo, nafikiri
ninaweza kuishi mpaka
miaka 60" (Mawaahib-ul-ladunniyyah, kilichoandikwa na Qastalani, Kitabu
cha I uk. 42).
Tamko hili ni la
ufunuo. Mtukufu Mtume s.a.w. hakusema lolote kwa kujikinai, bali alieleza
aliyoambiwa na Jibrili, Malaika wa Wahyi. Sehemu ya maana sana ya tamko hili ni
kwamba Isa aliishi miaka 120. Kwa maelezo ya Agano Jipya, Isa alikuwa yapata
miaka 32 au 33 hivi alipowambwa msalabani na "akapaa mbinguni."
Kama Isa kweli "alipaa" basi umri wake mpaka wakati wa Mtukufu Mtume
s.a.w. unakuwa karibu miaka 600, sio 120. Kama aliyoyapokea Mtukufu Mtume
s.a.w. kutoka kwa Jibrili ni ya kweli, Mtume s.a.w. kuwa mfuasi wa Musa
aliyewahuisha wafuasi wa Musa. Silsila ya Musa ilidumu mpaka muda aliopenda
Mwenyezi Mungu.
Hatimaye ulipofika wakati wa kukoma kwa silsila hiyo, Mwenyezi Mungu
aliwaachia wafuasi wa Musa na kuelekea dhuria
wa Ismail kuinua Nabii kwa ajili ya
kuwaongoza wanadamu. Kama sasa, aje Nabii wa silsila ya Musa kuwaongoza wafuasi wa
Mtukufu Mtume
s.a.w., itakuwa na maana (Mungu apishe mbali) kwamba Mwenyezi Mungu
ameamua kuikomesha silsila ya Mtukufu Mtume
s.a.w. kama alivyokomesha silsila ya
Musa, na ya kwamba mahala pake anaanzisha silsila mpya. Itakuwa na maana (Mungu apishe mbali tena) ya kwamba
nguvu ya kiroho ya Mtume Mtukufu s.a.w.
haina athari tena hivi kwamba
inashindwa kumpatia hata mfuasi mmoja nuru iliyo muhimu kwa kuhuishia na kuongozea wafuasi wake
tokana na mafundisho na mfano wake. Ole wao! juu ya kosa dogo sana linalotaka
kushusha hadhi yao wenyewe hawawezi kuvumilia; hawakubali dosari yoyote au upungufu
ndani yao. Lakini hawachelei kuingiza dosari na udhaifu kwa Mtukufu Mtume
s.a.w., na bado wanadai kuwa wapenzi wa Mtume s.a.w. Mtukufu. Yana faida gani
mapenzi ya kubwata kwa midomo tu lakini hayapatikani moyoni? Imani isiyofuatana
na vitendo ina maana gani? Kama Waislamu walimpenda kweli Mtukufu Mtume s.a.w.
wasingechekelea kufika kwa Nabii wa Kiyahudi kuja kuhuisha wafuasi wa Mtukufu
Mtume s.a.w. Ni nani anayeomba kwa jirani yake haja anayoweza kuikidhi nyumbani
mwake mwenyewe? Ni nani anayemwomba msaada mwenzake ambapo anaweza kujisaidia
mwenyewe? Masheikh wanaofikiri na kufundisha wafuasi wa Mtume s.a.w. kwamba Masihi
wa Nazaretiatafika mara ya pili wakati wa haja, wenyewe wanapita kiasi katika kulinda
uluwa wao hivikwamba katika majadiliano ya dini wangependa kuanguka kuliko
kukubali msaada kwa mwingine yeyote. Kama kuna msaada wowote, hawawi na furaha:
wanaumwa na kusema: "Je, tumeishiwa elimu sisi hivi kwamba tuhitaji msaada
wa wengine?" Lakini inapofika kwa Mtukufu Mtume s.a.w. wanakuwa wepesi mara
moja! Wanakuwa chapu sana kuamini na kufundisha ya kuwa zama wafuasi wa Mtukufu
Mtume s.a.w. wanapohitaji kuhuishwa, hawatapata uhuishaji huo kutokana na wafuasi
wa Mtukufu Mtume s.a.w. mwenyewe, sio kutokana na mvuto wa kiroho wa mwenyewe
Mtume s.a.w., bali kutokana na ukarimu wa Nabii wa silsila ya zamani, ambaye
hakupata chochote katika mafundisho ya Mtume s.a.w. Je, watu wamekuwa wafu na masugu
kiasi hiki? Je, wamepotewa na uwezo wote wa kufikiri na kuhisi? Wanahifadhi
heshima yao na uluwa wao wenyewe, lakini siyo kwa ajili ya Mwenyezi Mungu na
Mtume s.a.w. Wanaweza kuonesha ghadhabu na makasiriko kwa maadui zao binafsi,
lakini siyo kwa wale wanaomkosea Mungu na Mtume Wake? Tunaulizwa kwa nini
tunakataa kufika mara ya pili kwa Nabii wa Kiisraeli. Lakini tunaweza
tufanyeje? Hatuwezi kubadili mioyo yetu. Hatuwezi kuonesha mahaba yetu kwa
Mtukufu Mtume s.a.w. isipokuwa katika njia za kiasili. Heshima ya Mtukufu Mtume
s.a.w. ni penzi mno kwetu. Hatuwezi kufikiri kwamba kwa ajili ya kuhuisha wafuasi
wake, Mtume s.a.w. ahitaji msaada wa Nabii aliye mbali na yeye na kuwa mdeni
wake. Hatuwezi kufikiri hata kidogo kwamba siku ya Kiyama, wanadamu tokea wa
mwanzo mpaka wa mwisho kabisa watakapokusanyika mbele ya Mwenyezi Mungu, na
matendo na mafanikio yao yote yatatangazwa, Mtume s.a.w. atasimama na mzigo wa
deni la Masihi Mwisraeli, Malaika wakitangaza mbele ya wanadamu wote ya kwamba
wafuasi wa Mtukufu Mtume s.a.w. walipopotea, mfano wa kiroho wa Mtukufu huyu
mwenyewe ulishindwa kuwahuisha kwenye nguvu ya kiroho, kwa kumhurumia Mtukufu
Mtume s.a.w., Masihi wa Kiisraeli akajitupa kutoka peponi na kurudi ulimwenguni
kuwahuisha. Hatuwezi kuingiza fikara kama hii. Tungependa ndimi zetu zikatwe
kuliko kumkashifu Mtume s.a.w. kwa udhalilifu namna hii. Tungependa mikono yetu
ife ganzi kabisa kuliko kuandika jambo la namna hii kwa Mtukufu Mtume s.a.w. Mtukufu
Mtume s.a.w. ni mpenzi wa Mwenyezi Mungu. Nguvu yake ya kiroho haiwezi kamwe
kufutika. Yu Muhuri wa Manabii. Fadhili na baraka zake za kiroho hazimaliziki
kabisa. Hana haja kupata deni kwa Manabii wengine wowote na kudaiwa nao.
Manabii wengine ndio wanaodaiwa naye. Hakuna Nabii hata mmoja ambaye Mtukufu
Mtume s.a.w. hakutangaza ukweli wake mbele ya waliomkataa. Yalikuwa mafundisho
ya Mtukufu Mtume s.a.w. yaliyowaingiza mamilioni ya wanadamu katika imani juu
ya Manabii ambao walikuwa hawana habari nao. Kuna Waislamu milioni 80 katika India
(Wakati makala. Wachache miongoni mwao walitoka nchi za nje. Wengine ni wazawa
hasa wa nchi hii na walikuwa hawajapata kusikia juu ya Nabii yeyote yule.
Lakini tangu walipomwamini Mtukufu Mtume Muhammad, walianza kumwamini Ibrahimu,
Musa, Isa na wengine (amani ya Mungu iwe juu yao).
Kama wasingelikuwa Waislamu,
wangeendelea kuwadharau Manabii hawa, hata kuwatukana pia. wangeendelea
kuwafahamu kuwa walikuwa waongo kama vile Wahindu katika India wanavyoendelea kuamini
hivyo mpaka leo. Kadhalika Afghanistan, China na Iran. Wenyeji wa nchi hizi
hawakuwa na habari, hivyo hawakumkubali Musa na Isa kuwa Manabii. Ujumbe wa
Mtume s.a.w. ukaenea katika Wakati kitabu hiki kilipoandikwa
nchi hizi, na watu wake wakamwamini
Mtume s.a.w. na kila alichofundisha. Walianza kuwajua Manabii wengine na kuwaheshimu
kama Manabii wa kweli. Hivyo Mtukufu Mtume s.a.w. amewatwika mzigo wa deni
Manabii waliomtangulia wote. Ukweli wao ulikuwa haujulikani, Mtukufu Mtume
s.a.w. akaujulisha kwa watu. Mtukufu Mtume s.a.w. hana deni la mtu yeyote.
Fadhili na baraka za mafundisho yake lazima ziendelee milele. Kwa ajili ya
kuhuisha wafuasi wake hana haja ya msaada wa Nabii mwingine. Wakati wowote haja
ya namna hii inapotokea, Mwenyezi Mungu atainua mmoja wa wafuasi wake (Mtume
s.a.w.) awaongoze wafuasi wengine na kutengeneza kilichoharibika. Huyo atapata
kila kitu kutoka kwa Mtukufu Mtume s.a.w. Atajifunza kila kitu kutoka kwake.
Chochote awezacho kufanya, katika kuhuisha na kujenga upya, kitakuwa ni cha
Mtukufu Mtume s.a.w. mwenyewe. Chochote apatacho mwanafunzi kutoka kwa mwalimu,
hakika ni cha mwalimu. Mfuasi hawezi kutengwa mbali na Imam wake, na hivihivi
mwanafunzi hawezi kutengwa mbali na mwalimu wake. Mfuasi anayewaongoza wafuasi
wenzake atawiwa na Mtukufu Mtume s.a.w. na moyo wake na ubongo wake utakuwa
umejaa mapenzi yake. Kwa ufupi, kuja kwa Nabii wa zamani kwa ajili ya
kuhuishawafuasi wa Mtukufu Mtume s.a.w. ni matusi kwa Mtukufu Mtume s.a.w.. Tukio
kama hili linaweza kudhuru ukuu wa Mtukufu Mtume s.a.w. Kadhalika
litakadhibisha fundisho la Quran Tukufu lisemalo:
"Hakika Mwenyezi
Mungu Habadili yaliyoko kwa watu mpaka
wabadili yaliyomo
nafsini mwao" (13:12)
Hali ya kuona
fundisho hili la Quran, hatuna budi kukubali ama ya kuwa Mtukufu Mtume s.a.w.
(Mungu apishe mbali), amekuwa hastahiki ahadi ya Mwenyezi Mungu kwa kubadilika
hali yake, auya kwamba Mwenyezi Mungu mwenyewe amekhalifu ahadi yake. Kwa
wengine wote, mwendo wa Mwenyezi Mungu haukuwa kunyang'anya zawadi aliyokwisha
itoa; lakini kwa Mtukufu Mtume s.a.w. afanye vingine! Kuingiza fikira kama hii
kunafanya ukafiri. Kunafanya ama kumkataa Mwenyezi Mungu au kumkataa Mtume s.a.w.
Kwa sababu ya matokeo haya ya hatari tumechoka na itikadi kama hizi. Tunaamini
kwamba Masihi, ambaye kufika kwake kulitabiriwa na Mtukufu Mtume s.a.w. ni wa
kutokana na wafuasi wa Mtukufu Mtume s.a.w. Mwenyezi Mungu ana hiyari kumpa cheo
hiki mtu yeyote.
MASIHI NA MAHDI NI MTU MMOJA
Katika Hadithi za
Mtukufu Mtume s.a.w. inadhihirika pia ya kwamba Masihi Aliyeahidiwa ilikuwa awe
ni mfuasi wa Mtukufu Mtume s.a.w. Hadithi moja inatuambia kuwa:
"Mahdi siye ila
ni Isa". (Ibni Majah - Kitabul Fitan, Baab Shiddatuz-zaman)
Hadithi nyingine
inasema:
Mtakuwaje
atakapowafikieni mwana wa Mariam na kiongozi wenu atakuwa miongoni mwenu?"
(Bukhari, Kitabul-Anbiya, mlango Nuzuul Isa bin Maryam).
Hadithi hizi mbili
zinatoa shaka kabisa kwamba Masihi mwenyewe atakuwa Mahdi. Atawaongoza wafuasi
wa Mtukufu Mtume s.a.w. atatokana miongoni mwao, hatakuwa mtu wa nje. Kufikiri
kuwa Masihi na Mahdi ni watu wawili mbalimbali ni kosa. Ni kinyume na Ishara ya
wazi iliyomo ndani ya Hadithi:
"Mahdi siye ila ni Isa."
Inafaa waaminio wema kufikiri kwa makini
matamshi ya Bwana wao. Kama matamshi haya yanaonekana yanahitilafiana, ni juu yetu
kujaribu kuondoa hitilafu hiyo. Kama Mtukufu Mtume s.a.w. alisema upande mmoja,
kwamba Mahdi atadhihiri kabla ya Masihi, na kisha Masihi atajiunga na Mahdi na
kumfuata katika ibada; na upande mwingine, kwamba Masihi mwenyewe ndiye Mahdi,
tutafanyaje? Je, tukubali tamko moja na kukataa jingine? Au je, siyo wajibu
wetu kwamba tufikirie matamshi haya mawili kwa makini sana na kujaribu
kupatanisha moja na jingine? Matamshi mawili haya yanaweza kupatana kama
tulitumie moja kulitafsiri jingine. Inaonekana ya kwamba ahadi ya kudhihiri kwa
Mahdi ilibebwa ndani ya maneno yaliyodhanisha kwamba Masihi na Mahdi ni watu
wawili mbalimbali. Maoni haya yanasahihishwa na Hadithi isemayo kwamba
"Mahdi siye ila ni Isa". Hadithi hii inabainisha ya kuwa hiyo Hadithi
nyingine ni ya methali. Ina maana kwamba mfuasi wa Mtukufu Mtume s.a.w.
atatokea kwa ajili ya kuuhuisha ulimwengu, lakini hatakuwa na cheo cha Nabii.
Halafu ile ahadi ya kufika mara ya pili kwa Nabii Isa itatimia katika nafsi
yake na atajitangaza kuwa Masihi Aliyeahidiwa. Kwa hiyo, Hadithiinatuambia ya
kuwa Masihi Aliyeahidiwa ataanzia na kazi ya Mujaddid wa Kiislamu ambaye
atakuja pewa kazi ya Masihi. Vyeo viwili vitafuatana kwa mtu huyohuyo mmoja.
Bishara za kiungu mara nyingi hutumia methali. Ni mara chache sana zinapotumia vingine.
|
HADHRAT MAULVI NURUDDIN (RA), kHALIFATUL MASIH I |
Kama tafsiri yetu ya
Hadithi hizi si sahihi, basi kumebakia njia mbili tu kwa ajili ya atafutaye
ukweli: nazo zote ni za upuuzi na za hatari pia. Ama, tukubali ya kuwa ile
Hadithi inayoeleza kuwa Masihi na Mahdi ni mtu mmoja siyo Hadithi ya kweli, au,
tukubali ya kuwa Masihi na Mahdi ni watu wawili mbalimbali na ya kwamba dhamiri
ya Hadithi ni kuashiria hitilafu ya fadhila ya kiroho ya watu wawili hao.
Inaweza kuwa na maana ya kwamba Mahdi wa kweli atakuwa Masihi. Maana nyingine,
ni kwamba Mahdi atakuwa duni ya Masihi. Itakuwa kama kusema: "Hakuna
mwanachuoni ila fulani." Tusemapo hivyo, hatuna maana hasa kwamba hakuna
mwingine ajuaye. Bali tuna maana kwamba huyu fulani anajua sana. Kwa vyovyote
tafsiri hizi mbili ni za hatari. Moja inatutaka tuifanye kuwa ni ya uwongo
Hadithi ya Mtukufu Mtume s.a.w. iliyo ya kweli kwa kila mizani. Nyingine
inafahamisha kuwa Mahdi atakuwa si chochote mbele ya Masihi. Fikara hii itakuwa
kinyume na Hadithi zinazofundisha ya kuwa Mahdi atakuwa Imam na Masihi atakuwa mfuasi
anayesimama nyuma ya Imam katika sala ya jamaa. Hivyo njia zote mbili ni za
kipuuzi. Tafsiri zilizo bora ambazo tunaweza kuzitolea Hadithi hizi ni hizi tu
ya kuwa zinatabiri kuja kwa Mjumbe toka miongoni mwa wafuasi wa Mtukufu Mtume
s.a.w. Mjumbe huyu kwanza atadhihiri akiwa Mujaddid na baadaye atajitangaza kuwa
Masihi wa bishara. Mtu huyo huyo atakuwa Mahdi na Masihi pia. Hakutakuwa na
tafsiri yenye maana ya Hadithi hizi isipokuwa tafsiri hii.
NUZUUL SIO MAANA YAKE KUSHUKA KUTOKA MBINGUNI
Sababu ya mgogoro huu
ni kwamba kila mtu amepotezwa na neno nuzuul lililomo ndani ya Hadithi.
Maana yake halisi ni kushuka. Kwa hiyo watu wengi wamepotezwa na fikara kwamba
kwa vile Masihi imesemwa atashuka ni budi awe yule Masihi wa kwanza. Sasa basi,
ni kosa kufikiri ya kwamba neno nuzuul siku zote lina maana ya kushuka kutoka
juu. Neno nuzuul linaashiria tu ni ubora ulioje wa kitu kinachosemwa kuwa
kitashuka. Linatuambia kuwa kitu hicho cha kushuka kitakuwa chombo cha utukufu
na uwezo wa Mwenyezi Mungu. Vitu kama hivi vinasemwa kuwa huwashukia wanadamu
kutoka kwa Mwenyezi Mungu. Hii maana ya kushuka ni sawa na matumizi ya neno
hili ndani ya Quran Tukufu mahala pengi inasema:
"Kisha Mwenyezi
Mungu Akateremsha utulivu Wake juu ya Mtume Wake" (9:26).
"Kisha baada ya
huzuni Aliwateremshieni utulivu - usingizi ambao
ulifunika kundi moja
katika ninyi" (3:155).
"Na
Akawateremshieni wanyama wanne kwa jozi" (39:7).
"Hakika
Tumekuteremshieni nguo zifichazo aibu zenu na
mapambo; na nguo za
utawa ndizo bora. Hayo ni katika Ishara za
Mwenyezi Mungu ili
wapate kushika mauidha" (7:27).
"Na
Tukawateremshieni Manna na Salwa" (2:58).
"Na
tukakiteremsha chuma, chenye nguvu nyingi na manufaa kwa
watu; na ili Mwenyezi
Mungu Ajulishe anayemsaidia Yeye na
Mitume wake kwa siri.
Kwa yakini Mwenyezi Mungu ni Hodari,
Mwenye nguvu"
(57:26).
"Na kama
Mwenyezi Mungu Angetoa riziki nyingi kwa watumishi
wake bila shaka
wangaliasi ardhini, lakini Huiteremsha kwa
kipimo akipendacho.
Hakika Yeye kwa watumishi Wake ni
Mwenye habari, Mwenye
kuona" (42:28).
Kila mtu anajua ya
kuwa utulivu ni sifa ya akili ya mwanadamu na usingizi ni kazi ya ubongo wake.
Wanyama, nguo, mashamba, salwa, chuma na vitu vingine vinakuwa ardhini au
baadhi vinatoka ndani ya ardhi. Havishuki au kudondoka kutoka mbinguni. Wala kushuka
kwao kutoka mbinguni sio maelezo yaliyotumiwa na Quran Tukufu. Maelezo ya Quran
Tukufu yako wazi kabisa. Inasema:
"Na Akaweka humo
milima juu ya uso wake, na Akabarikia humo
na Akapima humo
chakula chake katika nyakati nne, ni sawa kwa waulizao" (41:11).
Katika aya hii,
Mwenyezi Mungu anaashiria kwamba maumbile yote ya kiasili na kuumbwa kwa mali
za namna mbalimbali kunahitaji elimu ya namna nyingi ili kufahamike. Elimu hii Mwenyezi
Mungu Huifunua sehemu sehemu. Sehemu imekwisha funuliwa, na sehemu itafunuliwa
wakati ujao. Kila swali jipya litatolewa na yote yatapata majibu yake. Lakini,
anasema Mwenyezi Mungu tumeeleza kuumbwa kwa maumbile ya kiasili na kuumbwa kwa
mali ya asili kwa njia ambayo watu wa nyakati zote (sawa na uwezo wao) watapata
ndani yake maelezo ya kweli na ya kutosheleza.
Hivyo, kutokana na
Quran Tukufu, inadhihirika kwamba vitu vyote vya kiasili hutoka kwa Mwenyezi
Mungu - vinatolewa na Mwenyezi Mungu - na tena havidondoki kutoka mbinguni.