Kwa jina la Mwenyezi Mungu, Mwingi wa Rehema, Mwingi wa Ukarimu
Sayyidna Hadhrat
Mirza Ghulam Ahmad a.s. (1835 - 1908 A.D.) Mwanzilishi Mtukufu wa Jumuiya ya
Waislamu wa Ahmadiyya ametumwa na Mwenyezi Mungu kwa niaba ya Mtukufu Mtume Muhammad
s.a.w. kuimarisha Dini ya Kiislam. Alidai kwamba yeye ni Imam Mahdi na Masihi
Aliyeahidiwa na Mtume Mtukufu Muhamamd s.a.w. na yeye ndiye kiongozi wa zama
hizi. Wafuasi wake walipatikana katika Afrika mashariki zama za uhai wake mnamo
mwaka 1896 A.D. Yeye aliimarisha na alifundisha dini ya Kiislaam, ile ile
iliyoletwa na Mtume Muhammad s.a.w. Baada yake makhalifa wake wamekuja sawa na
ahadi ya Mwenyezi Mungu na utabiri wa Mtume Mtukufu s.a.w. (Quran 24:56; Musnad Ahmad Jal. 4 uk. 273, Mishkat Bab
Indhar). Kazi za Jumuiya na nidhamu ya Jumuiya inapendeza, huduma ya kuimarisha
Dini ya Kiislam na kueneza mafundisho yake ni ya kutosheleza na hivyo ndivyo inavyotakiwa.
SHABAHA
YA KUANZISHA JUMUIYA MPYA
Sasa swali laweza
kuzuka kwamba, wakati Seyyidna Ahmad a.s. alitumwa kuimarisha Dini ya Kiislam,
ni kwa nini hakuungana na Waislam wengine, badala yake akaanzisha Jumuiya mpya
na kujitenga nao?
JIBU:
1.Utabiri
ulikuwepo wa Mtume Muhammad s.a.w. kwamba, wakati Waislamu watagawanyika
makundi 73, yote yataingia motoni isipokuwa kundi moja pekee ndilo litaenda
Peponi. (Jamee Tirmidhi Baabu Iftiraq). Aliulizwa
ni kundi gani hilo? Akasema Jamaat - yaani Jumuiya. Hivi ilikuwa lazima sawa na
utabiri, Jumuiya ile ingepatikana. Kwa nia hii na kwa idhini ya Mwenyezi Mungu
Seyyidna Ahmad a.s. alianzisha Jumuiya ya Waislamu wa Ahmadiyya.
2. Seyyidna Ahmad
a.s. ndiye Imam wa zama hizi. Jemedari wa jeshi la kiroho. Wakati yeye ameitwa
Imam ni lazima awe na wafuasi wake, Wakati yeye ni Jemedari wa jeshi la kiroho
lazima awe na jeshi la Dini. Yeye alitengeneza lile Jeshi la Mungu linaloitwa
Jumuiya ya Waislamu wa Ahmadiyya.
3. Wakati Sayyidna
Ahmad a.s. alitumwa kuhuisha Dini ya Kiislamu. Je, angefanya kazi peke yake?
Taratibu ya kazi inakuwa hivi kwamba kiongozi anaongoza na wafuasi wake na
wadogo wake wanafuata na wanafanya kazi. Sasa angalieni wakati Imam Mahdi
angetaka kuchapisha Qurani na Hadithi, angewaambia nani kazi hii? Wakati angetaka
kujenga msikiti na madrasa angemwambia nani? Wakati angetaka kuwaita watu
mkutanoni angewaita nani? Wakati angetaka kuwatuma wabashiri nchi za nje
angewatuma nani? Jibu la maswali hayo na mengineyo ni kwamba lazima awe na
wafuasi wake, wale ambao wanajulikana, wale ambao wanamfuata, na lazima wawe na
jina lolote.
JINA LA JUMUIYA
YA WAISLAM WAAHMADIYYA
Seyyidna Ahmad
a.s. kwa idhini ya Mwenyezi Mungu tarehe 23/3/ 1889 A.D. alianza kupokea Bait
za watu, na siku hadi siku watu maelfu walijiunga naye. Sasa swali lilikuwa
hili kwamba watambulike kwa jina gani? Kwa sababu Waislamu walianza kujiita kwa
majina mbalimbali. Kwa hiyo ilikuwa muhimu sana kwamba wafuasi wa Seyyidna
Ahmad wawe na jina maalumu. Seyyidna Ahmad a.s. ambaye alitumwa kwa niaba ya
Mtume Mtukufu Muhammad s.a.w. yeye alisema kwamba yeye hana chochote ila cha Muhammad s.a.w. na wafuasi wake si mbali na wafuasi wa
Mtukufu Mtume Muhammad s.a.w. Hivyo aliwaita wafuasi
wake kwa jina la Jumuiya ya Waislamu wa Ahmadiyya. Kwa sababu ya jina la pili -
Ahmad - la Mtume Muhammad s.a.w. Hapa ni vyema ieleweke vizuri kwamba jina la
Ahmadiyya si kwa sababu ya jina la Ahmad a.s. mwanazilishi wa Jumuiya. Bali ni
kwa sababu ya jina la pili la Mtume Mtukufu s.a.w. na muradi wake ni
Waislamu wa Mtume
Muhammad s.a.w. Si Waislamu wa katikati wala wa baadaye, kama vile wengine
wajiitavyo kwa jina la Sheikh fulani au mwalimu yeyote.
TOFAUTI BAINA
YA WAISLAMU WAAHMADIYYA NA WAISLAMU
WENGINE
Kama inavyoeleweka
kwamba, Waislamu wote wanayo dini moja yaani dini ya Kiislamu. Nguzo za dini ya
Kiislamu ni zilezile tano, na nguzo za imani ni zilezile sita. Wote wanamwamini
Mwenyezi Mungu na Mtume wake Muhamamd s.a.w. Lakini baadhi ya wakati inaonekana
hitilafu baina yao, ambapo wakati mwingine hitilafu hizi huwa kubwa mpaka baadhi
ya Waislamu wanawadhania vibaya wengine. Katika kitabu hiki tunachukua fursa
hii kueleza tofauti baina ya Waislamu wa Ahmadiyya na Waislamu wengine.
(1) Waislamu
Waahmadiyya tunaamini itikadi zile tu zinazoelezwa katika Qurani na Hadithi za
Mtume s.a.w. na tunakataa Bidaa na mambo yaliyobuniwa baadaye katika dini.
(3:86). Lakini Waislamu wengine wanaamini itikadi ambazo hazipatikani katika Qur'ani
na Hadithi na hii ni tofauti ya msingi. Kama mfano, Waislamu wengine wanaamini
kwamba:
(2) Waislam
wa Ahmadiyya tunaamini kwamba Mola wetu anazo sifa zote njema na hana
mabadiliko katika sifa yake yoyote, na kazi zote anafanya alizokuwa akifanya
zamani. Lakini Waislamu wengine wanaamini kwamba Mwenyezi Mungu haongei na mtu
yeyote siku hizi, hata kama mtu huyo awe na imani ya hali ya juu namna gani.
Kana kwamba Mungu wao siku hizi ni bubu na anakosa sifa moja ya kuongea.
(3) Waislamu
wa Ahmadiyya tunaamini kwamba Malaika ni viumbe wa Mwenyezi Mungu na wanafanya
kazi chini ya mwongozo wa Mwenyezi Mungu na kazi yao moja ni kuleta Wahyi (ufunuo)
kwa watu wema wa Mungu na bado wanaendelea kufanya kazi hii kama Mwenyezi Mungu
anavyoeleza katika Qurani Tukufu (41:31-32; 97:5-6). Lakini Waislamu wengine
wanasema kwamba Malaika hawafanyi kazi hii siku hizi bali wamekaa bure tu.
(4)
Waislamu wa Ahmadiyya Tunaamini kwamba Qurani Tukufu ni kitabu cha Mwenyezi
Mungu ambacho hakina shaka yoyote ndani yake wala hakuna mabadiliko wala
mafutiko katika Qurani, kwa sababu Mwenyezi Mungu ni mlinzi wake (15:10). Lakini
Waislamu wengine wanaamini kwamba aya kadhaa za Qurani tukufu zimebadilika na
zingine hazina athari zao na zingine zimefutwa, wanaziita kwa maneno ya Naasikh
na Mansuukh. Wengi wao hawaiamini Bismillahir Rahmaanir Rahiim kuwa ni
aya ya kwanza ya kila sura iliyowekwa juu yake.
(5) Waislamu
Waahamdiyya tunaamini kwamba Mitume wote wa Mwenyezi Mungu hawana dhambi
yoyote. Wote walikuwa wapendwa wa Mwenyezi Mungu na wenye utawa na uchamungu. Lakini
Waislamu wengine wanahitilafiana nasi, wanasema kwamba Mitume walikuwa na
dhambi kama vile kusema uongo, kuelekea kwa wanawake wengine na kadhalika.
Mifano mingi ya aina hii imetajwa katika tafsiri zao za Qurani hata mingine
kumhusu Mtume Mtukufu Muhammad s.a.w. (nau'udhu
billahi min dhaalika) Angalia Tafsiri
ya Jalalain maelezo ya Aya ya 24 Surat Yunus na pia maelezo ya aya ya 37
Suratul Ahzaab.
(6) Waislamu
wa Ahamdiyya tunaamini kwamba Hadhrat Isa a.s. (Yesu Kristo) alikuwa Nabii wa
Mwenyezi Mungu tu. Akiwa mwanadamu alikufa kifo cha kawaida kama walivyokufa
Mitume wengine wa Mwenyezi Mungu. (3:145 na 5:76) na hana sifa yoyote ya Mungu
kama kuishi bila kula chakula. Mayahudi walishindwa kumfisha msalabani (kumsulubu)
bali Mwenyezi Mungu alimsaidia na kumlinda na kifo cha msalaba na baada ya
mateso aliyoyapata msalabani alihamia nchi za Mashariki, akaishi huko na kufia
huko katika umri wa miaka 120 (Kanzul Ummal
Jl. 6 Uk. 160). Lakini Waislamu wengine wanawaunga mkono Wakristo kusema kwamba
Nabii Isa a.s. yu mzima mbinguni pamoja na Mwenyezi Mungu! Anaishi huko bila
kula chakula na bila mahitaji mengine ya kibinadamu na hana mabadiliko. Kana
kwamba ni Mungu wao mdogo.
(7) Sisi Waislamu wa Ahmadiyya tunaamini
kwamba utume ni neema na baraka ya Mwenyezi Mungu na neema zake zinahitajika
kwa mwanadamu kwa ajili ya maendeleo yake ya kiroho. Muongozo wake unahitajika
wakati ugonjwa wa kiroho unapotokea kama vile dawa inavyohitajika wakati
ugonjwa wa kimwili unapotokea. Hivyo sisi tunaamini kwamba utume katika dini ya
Kiislamu (kwa wafuasi wateule wa Mtukufu Mtume s.a.w.), unaendelea . Kazi ya
Mitume hao ni kufundisha na kueleza aya za Mwenyezi Mungu na kuelekeza kwenye dini
ileile iliyofundishwa na Mtume Muhammad s.a.w. (7:36). Kwa kuthibitisha hili
amekuja Hadhrat Ahmad a.s. Mwanzilishi wa Jumuiya ya Waislamu wa Ahmadiyya,
kutoka kwa Mwenyezi Mungu kwa niaba ya Mtume Muhamamd s.a.w. Hii ni kweli
kabisa kwamba dini ya Kiislamu imekamilika, sasa hakuna dini nyingine ila
Islam, na Mtume yeyote hana nafasi ya kuja kupinga au kubadilisha mafundisho ya
dini ya Kiislamu.Yeyote atakayetumwa lazima awe mtumishi na mfuasi wa Mtume
Mtukufu Muhammad s.a.w. Lakini Waislamu wengine wanasema kwamba Mtume Muhamamd s.a.w.
ni Mtume wa mwisho, na neema yoyote haitapatikana katika umati wake. Balaa,
fitina uwongo, udanganyifu, kugawanyika, madajjali, vyote vitapatikana lakini
dawa au mtu wa Mungu hatakuja.
(5) Ingawaje
Waislamu hawa wakati mwingine wanajipinga na kuhisia haja ya mtu wa Mungu pale
wanaposema kwamba Nabii Isa a.s. atashuka kutoka mbinguni kwa ajili ya
kuwaongoza Waislamu kwenye ushindi. Hawataki kabisa kwamba mwana (mfuasi) wa
Muhamamd s.a.w. achaguliwe kutuongoza lakini na wanamtegemea mwana wa Israeli
aje kuuhukumu umati wa Muhamamd s.a.w. Wao bila kujijua, maskini, wanaikana
nguvu ya kiroho ya kutakasa ya Mtume wao Mtukufu s.a.w.!
(8) Waislamu wa
Ahamdiyya tunaiamini ahadi ya Mwenyezi Mungu aliyowaahidi waaminio katika
Qurani (24:56) kwamba wale watakaoamini na kufanya vitendo vizuri watafanywa
Makhalifa katika ardhi.
Sawa na ahadi hii
ya Mwenyezi Mungu yeye tayari ameshaleta Makhalifa kati ya Wasialmu ili
kutimiza ahadi yake. Na kwa fadhili zisizo kikomo za Mwenyezi Mungu Jumuiya ya
Waislamu wa Ahamdiyya inaongozwa na Khalifa. Lakini Waislamu wengine wanasema
kwamba siku hizi hakuna Khalifa kati ya Waislamu na Waislamu wote wanaishi bila
kiongozi yeyote. Yaani umati hauna baba kama mwili usio na kichwa. Tunawauliza
Je, Mungu wao amesahau ahadi yake au wao wamekosa imani?
(9) Mtume Mtukufu
Muhamamd s.a.w. alitabiri kwamba baada ya kila miaka mia moja Mwenyezi Mungu
atamuinua Mujaddid (Mwenye kuimarisha dini) (Abu Daudi, Kitaabul Fitan). Tunaamini
kwamba sawa na utabiri wa Mtume Mtukufu s.a.w. katika kila karne ya Kiislamu
Mujaddid walifika na Mujaddid wa karne ya 14 ni Hadhrat Mirza Ghulam Ahmad a.s.
Waislamu wengine wameanzisha dhana kwamba Mwenyezi Mungu aliendelea kuwaleta
Mujaddid mpaka karne ya 13 lakini katika karne ya 14 Mwenyezi Mungu hakuleta
Mujaddid yeyote. Sasa ni karne ya 15 ya Kiislamu. (10) Mtume s.a.w. alitabiri
kwamba wakati wa upotevu wa umma wake Masihi na Mahdi atakuja kuwaongoza
Waislamu na kuleta ushindi wa dini ya Kiislamu. Sasa Waislamu Waahmadiyya
tunaamini kwamba katika wakati huu wa upotevu wa umma wa Mtume s.a.w. Mwenyezi
Mungu amemtuma Masihi Aliyeahidiwa na Imam Mahdi ambaye ni Seyyidna Ahmad a.s. Lakini
Waislamu wengine wanasema kwamba hii ni kweli upotevu namfarakano mkubwa
umetokea katika Waislamu, lakini kiongozi wa kidini, Imam wa Kiroho
hajapatikana. Ugonjwa umeenea sana lakini dawa haijapatikana. Kama waulizwe,
je, Mtume wenu alisema kweli, au Mungu wake hakutambua ahadi aliyowapa wafuasi
wake? Watajibuje!!!
(11) Sisi
Waislamu wa Ahamdiyya tunaamini kwamba dini ya Kiislamu ilikamilika katika
maisha ya Mtume Muhamamd s.a.w., na baada yake mtu yeyote hana ruhusa kuongeza
wala kupunguza chochote katika sheria za Kiislamu. Wakati tunatangaza dini
halisi bila bidaa yoyoteWaislamu wengine wanafikiri kwamba tunatangaza dini
mpya. Ilhali hawa jamaa wameifunika dini na takataka nyingi za bidaa. Hivyo wanapoelezwa
dini halisi ya Mtume Muhamamd s.a.w. wanafikiri kuwa ni dini mpya. Kwa mfano
mambo kama: (i) Khitima, (ii) Arobaini, (iii) Talasimu, (iv) Talaqini, (v)
Maulidi ya kupiga ngoma na kucheza dansi na kadha wa kadha, ilhali mambo haya yote
hayana msingi katika dini, si suna ya Mtume s.a.w. Mtukufu wala ya Masahaba
wake, Bali wametunga mambo haya baadaye kwa matamanio yao.
12. Sisi
Waislamu wa Ahmadiyya tunaamini kwamba Hadhrat Muhammad s.a.w. ndiye
Khaatamunnabiyyin. Yaani Mbora na Muhuri wa Manabii wote, na hatakuja Mtume
yeyote baada yake ambaye aje na dini mpya au afundishe jambo lolote kinyume cha
Sunna za Mtume s.a.w. Na tunaamini kwamba sasa daraja zote za kiroho
zinapatikana katika umati wake. Waaminio wake na wafuasi wake watachaguliwa kwa
kupewa neema zote.(4:70). Lakini Waislamu wengine wanasema kwamba wafuasi wa
Mtume Muhammad s.a.w. hawatapewa neema yoyote kutoka kwa Mwenyezi Mungu. Bali
Nabii Isa a.s. atakuja mara ya pili. Kwa njia hii sawa na jamaa hawa Nabii Isa
a.s. ndiye mwisho wa Manabii na si Mtume Muhammad s.a.w., kwa sababu Nabii Isa
a.s. sasa atakuja baada ya Muhammad s.a.w. na atafanya kazi ya utume baada ya
Muhammad s.a.w. Baadhi yao wengine kwa kuona ubaya wa imani yao hiyo wanajasiri
kiasi hiki kwamba wanasema Nabii Isa a.s. atakapokuja atanyang'anywa cheo chake
cha Utume. Sasa kila mtu anao uhuru wa kufuata imani yake. Kama wewe unaunga
mkono upande wa juu basi wewe ni Muislamu Waahmadiyya, wewe ni ndugu yetu, uko
wapi? Tunakutafuta. Na mtu ambaye anaunga mkono upande wa chini, anakuwa upande
wa hao Waislamu wengine. Pia kama wewe unakubaliana na mawazo ya Waislamu
wengine chini ya kila nukta iliyoelezwa hapo juu, tunakukaribisha tafadhali
uchunguze, uhakikishe kwamba ukweli uko wapi? Ili uweze kufuata Dini ya
Mwenyezi Mungu na njia iliyonyooka.
SWALI:
JIBU:
1. Mitume
wanachaguliwa na Mwenyezi Mungu na wanapewa madaraka na vyeo mbalimbali. Kwa
hiyo wakati wanapewa madaraka yoyote, inakuwa ni jukumu lao kutangaza. Basi
wanatangaza na wanadai madai yale wanayopewa na Mwenyezi Mungu.
2. Mitume
hawafunuliwi mambo yote katika siku moja, bali wanaendelea kufunuliwa maisha
yao yote. Basi jambo wanaloambiwa kwanza wanalitangaza kwanza, na jambo
wanaloambiwa baadaye wanalitangaza baadaye. Kwa mfano Qur'an Tukufu
iliteremshwa katika muda wa miaka 23.
3. Ulikuwepo
utabiri wa kuongeza madai: Imam Mahdi atadai kuwa Adam, Nuhu, Musa, Isa na
Muhammad s.a.w. na Maimamu wa Ahlul Bait. (Biharul Anwar Jl. 13 uk. Na. 33).
4. Kuongeza
ongeza madai ni sunna ya Mtume wetu Muhammad s.a.w
inayopatikana
katika Qur'an tukufu, Kwa hiyo Sayyidna Ahmad a.s. kwa sababu zilizotajwa hapo
juu amejaaliwa kufuata nyayo na sunna za Mtume Mtukufu Muhammad s.a.w. Madai
mbali mbali ya manabii katika Qur'an Tukufu Mtume Muhammad s.a.w.
1. Na siye
Muhammad ila Mtume tu. (3:145).
2. Nabii aliye
Ummi (7:158).
3. Nabii (33:2).
4. Shahidi
(33:46).
5. Mubashshir
(Mtoaji wa habari njema) (33:46).
6. Nazir
(Muonyaji). (33:46).
7. Dai ila llah
(Muitaji kwa Allah) (33:47).
8. Siraajumunira
(Taa itoayo nuru (33:47).
9. Rehema kwa
walimwengu (21:108).
10.
Khaatamunnabiyyin (Muhuri wa Manabii) (33;41).
11. Muzammil
(Mwenye kujifunika nguo) (73:2)
12. Mudaththir
(Mwenye kuvaa) (74:2).
Madai, sifa na
vyeo vya Mtume Mtukufu Muhammad s.a.w. vimetajwa vingi mno katika Qur'an Tukufu
na katika Hadithi pia. Katika hadithi moja Mtume Mtukufu s.a.w. amesema: Mimi
ni Muhammad, Ahmad, Mahi, Hasher na Aaqib. (Bukhari). Vilevile manabii wengine
pia walipewa vyeo mbalimbali. Tunawataja baadhi
yao pamoja na vyeo vyao.
Itaendelea...
3 comments:
Maashaallah, jazakaallahu la'aziz. Ni maelezo mazuri yenye ushahidi unaothibitika na tunamuomba Allah aendelee kutujaalia neema Islam ahmadiyya na atuongoze katika njia nyoofu. Amiim.
Safi sana nime soma na nime elewa
Waislamu mnapingana wenyeqe,OK karibun kwa yesu mbatizwe
Post a Comment